Habari Mpya

Friday, August 15, 2014

WAANDISHI TUEPUKE HAYA KWENYE UTANGAZAJI

Vicky Ntetema mwandishi mahiri wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).



Na Frank Bruno.

Tanzania tumejaliwa kuwa na vyombo vya habari vingi sana nikimaanisha Redio, Runinga pamoja na magazeti. Moja ya sehemu inayo sisitizwa kwa watangazaji na waandishi kuwa na mtindo binafsi wa kutangaza ni kwenye somo la uandishi wa utangazaji (broadcast journalism), kwa kurejea vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari kwa mfano Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro  kitengo hiki kipo chini ya  Mwezeshaji Ndg Hashim Gulana. Somo ambalo wanafunzi wengi wa uandishi wahabari, wanalipendelea zaidi kuliko masomo mengine, wapo ambao mara ya kwanza walipo wasili tu chuoni hapo, karibu wanafunzi wengi walionesha kupendelea zaidi somo la utangazaji tu bila masomo mengine.





Baraka wa Kitenge akipewa maelekezo na mtangazaji mkongwe Charles Hillary jinsi wanavyotayarisha habari zao BBC alipotembelea ofisi za BBC.


Utafiti umebaini, wanafunzi wengi, wanapendelea sauti zao zisikike zaidi kwa wasikilizaji. Pia wengi wao wanataka wajulikane na wawe maarufu kama watangazaji wa redio ambazo zilitangulia kurusha matangazo yake, na karibu wote wanatamani wakafanye kazi katika mkoa wa Dar es salaam ambako kuna idadi kubwa ya vyombo vya habari.
Tunapo angalia redio na madhumuni yake tunaona ni chombo kinacholusha matangazo yake ili kuwasiliana na watu, kwa kuburudisha, kuhabarisha na kufundisha     mambo mbalimbali. Kwa kutaja machache redio za sasa zipo kwa ajili ya maongezi sana maarufu kama ‘Zogo’, ambapo kwa sasa ukitaka uajiliwe redioni unaulizwa una ‘zogo’? Yani una mudu kuongea sana? Huu ni mtindo mpya unao shika kasi katika redio zetu. Tatizo lililopo, baadhi ya waandishi wakikosa cha kuongea, hudhubutu hata kuongea matusi, na kubadilisha studio kua kijiwe cha kusutana.
Kama mtangazaji ni vema ukaingia na muongozo (script) ambao itakusaidia kukuongoza na kutoongea vitu visivyo hitajika kwa wasikilizaji. Wasikilizaji wana hitaji kujifunza mambo mengi na changamoto kupitia vyombo vya habari. Lakini kutokana na uvivu wa baadhi ya waandishi hapa nchini wa kutofuatilia mambo yanayoibuka kila wakati duniani unatufanya tuingie kazini kwa kukosa cha kuongea na matokeo yake kuanza kuendesha vipindi vya udaku.
Osea Mchopa mwanafunzi wa ngazi ya stashaada katika chuo cha uandishi wa habari morogoro anasema wanachuo wengi katika vyuo vya uandishi wa habari wanatabia ya kuiga sauti za watangazaji wengine sio uhalisia wao na ndio maana wanashindwa kuwa wabunifu. “ukifuata misingi uliyofundishwa ndio kigezo tosha cha kukufanya uweze kufanikiwa” aliongeza Mchopa.
 Pia Paskalina Kidyara makamu wa rais serikali ya wanafunzi katika chuo cha uandishi wa habari Morogoro aliongeza kwa kusema kuwa lazima waandishi wawe wabunifu ingawa tunaweza kuiga namna ya utangazaji lakini sio sauti.  

“Haikatazwi kuwa na mtu wako anaekuvutia (role mode) katika utangazaji ila jambo la msingi lazima uwe wapekee katika utangazaji” alisema Hashim Gulana mkufunzi katika chuo cha uandishi wa habari morogoro
Tunawaona waandishi wakongwe kama Tido Muhando, George Njogopa, Vicky Mtetema, kwa hao wachache na wengine wengi, walikuwa wanafanya vipindi makini vilivyo waletea maendeleo makubwa, mpaka kufanya kazi katika vyombo vya habari maarufu duniani kama BBC & DW.
Tuking'ang'ania kufuata aina fulani ya utangazaji wa watangazaji wetu wa kisasa hapa nchini hakika hatuwezi kuimalisha misingi ya utangazaji yenye radha na utamaduni wa kitanzania kama ilivyokua hapo zamani enzi za kina Charles Hillaly, Julius Nyaisanga, Harima kiemba, Karim Besta na wengine wengi.
Waandishi wengi huujisahau na mara tu wanapomaliza masomo yao na kuanza na kuingia rasmi kwenye tathnia ya utangazaji huegemea zaidi kwenye upande wa burudani hasa ya muziki maarufu kama bongo fleva. Hakuna mitaala inayo fundisha waandishi waende wakapige miziki, ingawa kuburudisha ni sehemu ya wajibu wa redio. Kuna habari nyingi sana vijijini na sehemu mbalimbali tunaweza kutengeneza habari ambazo zina tija ndani ya jamii kuliko burudani.
Tasinia ya habari inalenga zaidi katika kuinufaisha jamii yake katika nyanja mbalimbali za kimaisha, kwa kutegemea waandishi walio wabunifu na wenye kujitoa zaidi kwa jamii.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: WAANDISHI TUEPUKE HAYA KWENYE UTANGAZAJI Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top